Na Paul Christian,Ulyankulu.
Mzee Solomoni Kazwika Milambo ni mmoja wa wazee
wachache wa ukoo wa Mtemi mashuhuri Milambo ambaye anaishi katika kijiji
Usigala barabara ya 44 Ulyankulu mkoani Tabora.
Kijiji hicho cha Usigala kipo kwenye eneo ambalo
linajulikana kama Ikonongo wakati wa utawala wa Mtemi Milambo.
Mzee huyo amezaliwa siku ya Jumatatu asubuhi ya
tarehe 18, Julai mwaka 1945 na sasa ametimiza umri wa miaka 70.
Mnamo tarehe 28 Novemba, 2015 mzee Solomoni
anakutana wa jopo la waandishi wa habari na kufanya mahojiano maalum kuhusu sifa za mtu anayepewa Utemi katika ukoo wa
Mtemi Milambo.
Mzee huyo alisema, “Sisi kupewa Utemi inatokana na
jinsi mtu alivyozaliwa au unabii unasemaje kuhusu mtu huyo.”
Alisema katika ukoo wa Milambo kabla ya Milambo
hajazaliwa alianza Sibuga ambapo alipozaliwa ilishuka nyota moja, babu yake na
Milambo aliyejulikana Kasele Muhofu aliongea akiwa bado tumboni mwa mama yake
na ndio maana aliishi miaka 300, (1520-1820).
Mzee Solomoni alifafanua, “halafu alifuata
shangazi Kibete alizaliwa akiwa malkia mwenye ziwa “titi moja” la mkono wa
kushoto.”
“Mimi mwenyewe kabla ya kuzaliwa niliongea nikiwa
tumboni mwa mama yangu na sikunyonya maziwa ya mama.” Aliongeza mzee huyo.
Mzee Solomoni alibainisha kuwa katika ukoo wa
Milambo, mtu anayekabidhiwa mikoba ya Utemi ni lazima azaliwe kimaajabu au kuwe
na unabii juu yake.
Alifafanua kuwa ikitokea akasimikwa Utemi mtu
asiyetokana na maajabu au maelekezo maalumu hawezi kumaliza miezi miwili au
mitano.
Siku hiyo ya Novemba 28, 2015, mzee Solomoni
aliongoza jopo la wazee wa ukoo wa Milambo katika zoezi la kimila la kumsimika
mbunge wa jimbo jipya la Ulyankulu John Peter Kadutu kuwa Mtemi.
Akizungumzia tukio hilo mzee huyo alisema kabla ya
kumsimika mheshimiwa Kadutu nilioteshwa namna ya kumfanyia hivi na vila na kama
nisingeoteshwa leo mvua isingenyesha.
Mzee Solomoni aliongeza “ndio maana mvua ilianza
kunyesha kuanzia saa tatu asubuhi hadi muda ule tunafanya tambiko la kimila la kumsimika mheshimiwa Kadutu.”